Ubora wa Maji

TATHMINI YA UBORA WA MAJI

Tathmini ya ubora wa maji ni muhimu kwa kuhakikisha maji ni salama kwa matumizi ya binadamu na kudumisha afya ya mazingira. Na zoezi hilo hufanyika kila baada ya robo ya mwaka, katika maeneo mbalimbali ya kwenye vyanzo vya maji yaliyoainishwa ndani ya eneo la Usimamizi wa Bonde katika Mkoa wa Tanga, Kilimanjaro na Arusha, Manyara (Simanjro na Kiteto). Vipimo vinahusisha vigezo vya Kimwili (Physical), Kikemikali (Chemical) na Kibaolojia (Biological) kwa kulinganisha na viwango vya kitaifa na kimataifa vya ubora wa maji, kwa lengo la kubaini hali ya maji kwa matumizi ya Kijamii, Kiuchumi na Kimazingira.Tathmini ya ubora wa maji katika maeneo husika inahusisha uchambuzi wa maji kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo Mito, Chemichemi, Mabwawa (dams), Maziwa (lakes), Visima virefu (Bore Hole) na vifupi (Shallow wells). Aidha, tathmini inajumuisha pia uchunguzi wa maji taka ya viwandani (industrial effluents) na Maji machafu ya manispaa (Municipal Effluents) baada ya kutibiwa ili kujiridhisha na ubora wake kabla ya kutiririshwa kwenye mazingira. Hatua hizi ni muhimu ili kuhakikisha maji yanayozalishwa, kutumika na kurejeshwa kwenye mazingira yanabaki salama na endelevu kwa matumizi ya sasa na ya baadaye.

Kwa ujumla, ubora wa maji unatofautiana kulingana na eneo na matumizi ya ardhi ndani ya eneo husika. Maeneo ya ukanda wa chini hupokea mtiririko unaobeba athari za matumizi ya ardhi kama makazi, kilimo na shughuli za kiuchumi, jambo linalosababisha mabadiliko makubwa zaidi ya kikemikali na kibaolojia. Hali hii huakisi athari za mkusanyiko wa uchafuzi (cumulative impacts) kadri maji yanavyosafiri kutoka ukanda wa juu kuelekea maeneo ya ukanda wa chini.

Ofisi ya Maji Bonde la Pangani inatoa wito kwa wananchi wote kuacha mara moja shughuli zozote zinazochangia uchafuzi wa vyanzo vya maji, ikiwemo utiririshaji holela wa majitaka, utupaji wa taka kwenye mito na chemchemi, kilimo ndani ya maeneo ya hifadhi ya vyanzo (buffer zones), ukataji miti, uvuvi haramu wa kutumia sumu, uchimbaji madini, pamoja na shughuli za mifugo ndani ya vyanzo na kandokando ya mito bila udhibiti.

Kwani shuguli hizo huongeza mzigo wa uchafuzi, kupunguza ubora wa maji na kuvuruga usawa wa ikolojia wa mfumo wa maji. Matokeo yake, maji hayo huwa hayafai kwa matumizi ya kibinadamu bila matibabu ya kina. Pia, husababisha kuongezeka kwa gharama za matibabu ya maji (water treatment costs) ili kuondoa uchafu wa kikemikali na kibaolojia kabla ya kusambazwa kwa jamii.

Tunasisitiza umuhimu wa kuhifadhi maeneo ya vyanzo vya maji, kupanda miti katika maeneo ya recharge zones na kufuata miongozo ya usimamizi wa mazingira ili kulinda ubora wa maji na ustawi wa kiasili wa mfumo wa mazingira (ecological integrity) ya vyanzo vyetu. Ushiriki wa jamii ni nguzo muhimu katika kudhibiti uchafuzi na kuimarisha uwezo wa kujisafisha wa asili (self-purification capacity) ya mifumo ya maji. Kulinda vyanzo vya maji ni jukumu la kila mwananchi. Kwa kushirikiana, tunaweza kuhakikisha upatikanaji wa maji safi, salama na endelevu kwa kizazi cha sasa na kwa vizazi vijavyo, sambamba na kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi yanayotegemea rasilimali hii muhimu.