Maji chini ya Ardhi

Maji Chini ya Ardhi

Majichini ya Ardhi ni yale maji yanayopatikana chini ya uso wa Dunia ambayo hutunzwa katika nyufa, udongo, mchanga na katika miamba ambayo ina sifa za kutunza maji ambayo hujulikana kama miamba maji (aquifers). Maji haya tunaweza kuyapata kwa njia ya kuchimba visima na chemchemi ambazo ambazo hutirirsha maji kutoka chini ya ardhi kwa nguvu asilia za mgandamizo wa maji zinazotekea katika miamba maji.

Maji chini ya ardhi katika maeneo ya Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro hupatikana katika miamba ya volkeno, kwa Mkoa wa Tanga hupatikana katika miamba tabaka na katika Mkoa wa Manyara (Simanjiro) maji chini ya ardhi hupatikana katika miamba ya volkeno na tabaka.

Upatikanaji wa Maji chini ya Ardhi

 Maeneo yote haya yana visima vifupi (mita 3 hadi 15), visima vya kati (mita 16 hadi 50) na visima virefu (mita 50 hadi 300). Visima virefu na vyenye uwezo wa kutoa maji kati ya lita 50,000 na lita 800,000 kwa saa vimechimbwa katika maeneo ya mkoa wa Arusha (Shamba la mbegu, Valesca Mbuguni na Tengeru kwa ajili ya matumizi ya mradi wa Maji AUWSA), mkoa wa Kilimanjaro (Majimoto – Hai (AUWSA), Kahe Miwaleni - Moshi (TPC), Sterling - Same (Kwa ajili ya Mji wa Same)) Mkoa wa Tanga (Mwakileo - Tanga(Kwa ajili ya Usambazaji wa Maji unaofanywa na Tanga-UWASA) Mjini na Mwera - Pangani(Kwa ajili ya Usambazaji wa Maji unaofanywa na RUWASA-Pangani). Kisima chenye uwezo wa kutoa lita 800,000 kwa saa kinapatikana katika kidakio cha kahe – miwaleni kilichochimbwa ndani ya shamba la miwa la TPC.

Ufuatiliaji wa mwenendo wa Maji chini ya Ardhi katika Bonde unafanyika kupitia visima 102 vya uchunguzi vilivyoko katika Bonde, ambapo kati ya hivyo visima 11 ni vya Bonde la Pangani, visima 65 vya TPC, 24 vya Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela  na visima 2 vya Halmashauri ya Jiji la Tanga. Mgawanyo wa visima hivi kwa Mikoa ni kuwa; visima 27 viko katika Mkoa wa Arusha, 70 Mkoa wa Kilimanjaro  na visima 5 Mkoa wa Tanga.

Vipimo vilivyochukuliwa kwa miaka mitano iliyopita (2017 –2021) vinaonyesha kuna mabadiliko ya kupanda na kushuka kwa maji chini ya ardhi kwa vipindi vya mvua na jua kwa wastani wa mita 1.