Uzinduzi wa Jumuiya...
Uzinduzi wa Jumuiya 2 za Usimamizi wa Rasilimali za Maji na Uhifadhi wa Mazingira Kidakio Kidogo cha Mto Ungwasi na Mto Tarakea-Rongai, Wilaya Rombo
21 Mar, 2026 07:00AM-10:30PM Wilaya ya Rombo-Ukumbi wa Gosheni
Uzinduzi wa Jumuiya 2 za Usimamizi wa Rasilimali za Maji na Uhifadhi wa Mazingira Kidakio Kidogo cha Mto Ungwasi na Mto Tarakea-Rongai, Wilaya Rombo

Bodi ya Maji Bonde la Pangani kwa kushirikiana na Shirika la WWF, KINAPA na Halmashauri ya Wilaya ya Rombo wamewezesha Uundwaji wa Jumuiya mbili (2) za Watumia Maji ambazo ni Jumuiya ya Watumia Maji na  Uhifadhi wa Mazingira Kidakio Kidogo cha Mto Ungwasi (JUWAMAKIUNGWA); na Jumuiya ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji na Uhifadhi wa Mazingira Kidakio Kidogo cha Tarakea-Rongai (JUWAMAKITARO).

Uzinduzi rasmi wa Jumuiya hizo ulifanyika tarehe 19 Machi 2026 katika Ukumbi wa Gosheni uliopo Halmashauri ya Wilaya Rombo ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya Rombo Mhe. Raymond Mwangwala.

Lengo kuu la kuanzishwa kwa Jumuiya hizi ni kuwaunganisha watumia maji na wadau wengine ili kwa pamoja waweze kupanga, kusimamia, kulinda, kuhifadhi na kuendeleza Rasilimali za Maji katika eneo la Kidakio Kidogo cha Mto Ungwasi na Tarakea-Rongai kwa manufaa ya wakazi wake na walio nje ya eneo ili kupunguza umasikini.

Mpaka sasa jumla ya Jumuiya 24 zimeshaundwa na kusajiliwa katika Bonde la Pangani na kukamilika kwa Jumuiya hizi mbili zitafanya jumla ya Jumuiya kwenye Bonde la Pangani kuwa 26  na kati ya hizo, Jumuiya 10 zipo katika Mkoa wa Kilimanjaro. Hii inatoa fursa kwa Mkoa wa Kilimanjaro kusimamia vyanzo vya maji kwa ukaribu kwa kuwa Jumuiya hizi zipo katika ngazi ya Jamii na hivyo zinafanya kazi moja kwa moja na watumia maji walioko kwenye jamii husika.

Jumuiya ya Watumia Maji na Uhifadhi wa Mazingira Kidakio Kidogo cha Mto Ungwasi

Inajumuisha Tarafa 3, Kata  10 yenye jumla ya Vijiji 20 na Mitaa 3. Kata Kumi (10) za Kelamfua Mokala, Shimbi, Makiidi, Ushiri Ikuini, Mrao Keryo, Kirwa, Katangara, Mengeni, Olele na Aleni ambapo ndani ya Kata hizo kuna jumla ya Vijiji na Mitaa Ishirini na mbili (22) vya Kelamfua, Ibukoni, Mokala, Shimbi Masho, Shimbi Mashami, Makiidi, Maharo, Ushiri, Ikuini, Ubaa, Mashuba, Keryo, Mrao, Momwe, Kirwa, Keni, Kiraeni, Katangara, Mrere, Mengeni Kilema, Mengeni Kitasha, Kooti na Machame Aleni.  

Jumuiya ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji na Uhifadhi wa Mazingira Kidakio Kidogo cha Tarakea- Rongai

Inahudumia Tarafa 3, Kata 10 yenye jumla ya Vijiji 28 na Mitaa 4 ambazo ni Kata Kumi (10) za Motamburu Kitendeni, Tarakea Motamburu, Nanjara, Reha, Ubetu Kahe, Kitirima, Kingachi Kirongo Samanga, Marangu Kitowo, Kisale Msaranga. Na Vijiji (32) zilizopo Kando kando ya Mto Rongai – Tarakea ambazo ni vijiji vya Kamwanga, Endonet, Rongai, Nalemuru, Kikelelwa, Mbomai, Msangai, Kibaoni, Nayeme, Urauri, Nessae, Ture, Kahe, Ngaseni, Ubetu, Wama, Lesoroma, Msinga, Kwalakamu, Kingachi, Leto, Usongo, Kirongo chini, Kirongo Juu, Samanga, Kiwanda, Sangasa, Marangu Kitowo, Kisale, Msaranga na Mahorosha. Kila kijiji kilitoa wawakilishi kutoka makundi mbalimbali za watumia maji ikiwemo kikundi cha mazingira, wakulima na wamwagiliaji, wafugaji, wavuvi, BMU na maji majumbani

Jumuiya hizi zinaongozwa na Kamati ya uongozi wa watu sita (6) unaojumuisha Mwenyekiti, Makamu mwenyekiti, Katibu, Mhazini na wajumbe wawili (2) waliopatikana kwa mujibu wa sheria na kanuni za Jumuiya kama ilivyoainishwa kwenye Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Na.11 ya Mwaka 2009.

  1. Mchakato wa kuunda Jumuiya ya Watumia Maji na Uhifadhi wa Mazingira Kidakio Kidogo cha Mto Ungwasi.

Bodi ya Maji Bonde la Pangani kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Rombo pamoja na Shirika la Wanyama Pori (WWF) na KINAPA iliwezesha mchakato wa uanzishwaji wa Jumuiya ya Watumia Maji na Uhifadhi wa Mazingira Kidakio Kidogo cha Mto Ungwasi na Tarakea-Rongai kwa ajili ya kusimamia na kutunza vyanzo vya maji pamoja na mazingira yake yote.

Mchakato wa Uundaji wa Jumuiya za watumia maji ulipitia hatua mbalimbali kwa kuzingatia muongozo wa Uundaji wa Jumuiya za Watumia maji, na katika hatua hizo wananchi, viongozi na wadau mbalimbali walishirikishwa kwenye maeneo yao kupitia mikutano ya hadhara ya Vijiji/Mitaa na wakati wa uhamasishaji huo wananchi na Wadau katika maeneo hayo waliainisha changamoto mbalimbali zinazokabili vyanzo vya maji. Kwa kuwa isingekuwa rahisi kwa wananchi wote kushiriki kwa pamoja walichagua wawakilishi ambao walijadiliana na kutengeneza Katiba za Jumuiya hizo itakayowaongoza katika kusimamia vyanzo vya maji na kutatua changamoto mbalimbali vilivyoainishwa.

Jumuiya hizi zitatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia katiba ya Jumuiya ili kuhakikisha yafuatayo yanafanyika;

  1. Kuhifadhi Mazingira hususani Usimamizi wa Rasilimali za Maji kwenye vyanzo vya maji
  2. Uelimishaji Wadau na Wananchi juu ya usimamizi wa pamoja wa rasilimali za maji na mazingira
  3. Jumuiya kuchukua hatua kwa waharibifu wa mazingira katika vyanzo vya maji na kingo za mito
  4. Kutatua migogoro zinazohusu matumizi ya maji baina ya makundi mbalimbali
  5. Jumuiya kufanya ufuatiliaji wa masuala mbalimbali yanayohusu usimamizi wa rasilimali za maji kama vile, uchepushaji holela wa maji kutoka kwenye vyanzo vya maji, ukataji hovyo wa miti katika vyanzo vya maji, uchimbaji madini kwenye vyanzo vya maji na shughuli zingine za kibinadamu zinazochangia uharibifu wa vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla

Wakati wa hotuba ya Uzinduzi, Mgeni Rasmi alisema kuwa ‘’Uzinduzi wa Jumuiya una lengo la kuhabarisha umma kuhusu uwepo wa chombo hiki kisheria ili wadau wote waweze kukifahamu na kukipa ushirikiano stahiki katika jukumu kubwa walilokabidhiwa kutekeleza kwa niaba yetu sote’’.

Alisisitiza kuwa  ‘’Baada ya uzinduzi huu ni matumaini yangu kuwa viongozi wa ngazi mbali mbali, wadau na wananchi wote mtashirikiana na Jumuiya hizi katika kutunza mazingira na kulinda vyanzo vyetu vya maji  ikiwemo Kidakio Kidogo cha Mto Ungwasi, Tarakea -Rongai na vijito vyake kwani hatua hii ni muendelezo wa utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita ambayo imetoa msisitizo maalumu kuhusiana na utunzaji wa vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla. 

Alitoa mfano wa hivi karibuni ya  Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipoadhimisha kumbukizi ya siku yake ya kuzaliwa tarehe 27 Januari 2026 kwa kupanda miti katika maeneo ya Bungi Kilimo na Kizimkazi, Zanzibar. Katika tukio hilo, Mheshimiwa Rais alisisitiza kuwa upandaji na utunzaji wa miti ni hatua muhimu katika kulinda misitu, kurejesha uoto wa asili, kuhifadhi bayoanuai na kuimarisha uwezo wa Taifa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho. Aliongeza kuwa ni muhimu kujenga na kuendeleza utamaduni wa kulinda na kuhifadhi mazingira na kuurithisha kwa watoto wetu, kwani mtoto anayepanda na kutunza mti akiwa mdogo hukua akiwa na upendo wa mazingira na fikra za kulinda maliasili za Taifa letu.

Vilevile uzinduzi wa Jumuiya hizi ulienda sambamba na maadhimisho ya Wiki ya Maji Kitaifa ambapo kilele chake ni tarehe 22 Machi 2026 Mkoani Morogoro. Kauli mbiu ya Maadhimisho hayo kwa mwaka huu 2026 inasema ‘Maji na Jinsia’

Uzinduzi wa Jumuiya hizo uliambatana na makabidhiano ya vitendea kazi kama vile pikipiki, samani za ofisi, mizinga ya nyuki na vitendea kazi vingine.

#KAZI NA UTU TUNASONGA MBELE

‘’UTUNZAJI WA VYANZO VYA MAJI NI JUKUMU LETU SOTE’’