TAARIFA YA UFAFANUZI WA UTABIRI WA HALI YA MVUA KWA MWEZI OKTOBA KWA MWAKA 2025 KATIKA MAENEO YA BONDE LA PANGANI

WIKI YA KWANZA
Kwa wiki hii katika vidakio vya Bonde la Pangani kunatarajiwa kuwa na hali ya ukavu kwa ujumla. Hali kadhalika baadhi ya maeneo ya Kidakio cha Msangazi ikijumuisha maeneo yaliyopo katika Mkoa wa Tanga (Wilaya ya Handeni na Pangani), Kidakio cha Ruvu na Kikuletwa (maeneo ya Mkoa wa Kilimanjaro hasa maeneo ya Wilaya ya Moshi, Siha na Hai) yanatarajiwa kuwa na mvua nyepesi zenye wastani wa chini ya Milimita Kumi (10) kwa maeneo machache huku maeneo mengi yaliyosalia katika vidakio kuwa makavu.
• WIKI YA PILI
Kwa wiki hii katika Kidakio cha Mkomazi haswa maeneo ya Wilaya ya Same, Korogwe na Kidakio cha Umba Wilaya Lushoto katika maeneo ya Mlalo na Bumbuli; Kidakio cha Luengera na Zigi haswa maeneo machache ya Wilaya ya Muheza pamoja na Kidakio cha Kikuletwa kuna matarajio ya kupata mvua za wastani wa chini ya milimita 10 kwa maeneo mengi huku Kidakio cha Pangani Mkuu na Msangazi kukitarajiwa kuwa na hali ya ukavu haswa katika Wilaya za Same kwa Mkoa wa Kilimanjaro na Wilaya za Korogwe na Handeni kwa Mkoa wa Tanga.
• WIKI YA TATU
Kwa wiki hii katika Vidakio vya Pangani Mkuu haswa maeneo yaliyopo katika Wilaya za Korogwe, Mkoa wa Tanga na Simanjiro Mkoa wa Manyara, Kidakio cha Umba maeneo ya Wilaya ya Lushoto pamoja na Kidakio cha Msangazi hususani maeneo ya Wilaya za Handeni na Pangani kunatarajiwa kuwa na hali ya ukavu kwa ujumla. Halikadhalika baadhi ya maeneo ya Kidakio cha Mkomazi na Kikuletwa katika maeneo yalioko Mkoa wa Arusha na Kilimanjaro yanatarajiwa kuwa na mvua nyepesi zenye wastani wa chini ya Milimita Kumi (10 mpaka 20) kwa maeneo machache.
• WIKI YA NNE
Kwa wiki hii kuna matarajio ya kupata mvua kubwa kiasi cha wastani wa Milimita 50-200 kwa ukanda wa Mashariki mwa Bonde haswa katika maeneo mengi ya Mkoa wa Tanga katika vidakio vya Mkulumuzi na Zigi hususani maeneo ya Wilaya ya Mkinga na Muheza Mkoani Tanga pamoja na Kidakio cha Luengera na Umba. Hata hivyo maeneo mengine machache ambayo yanayotarajiwa kupata mvua kubwa yameweza kutabiriwa katika Kidakio cha Kikuletwa na Ruvu hususani katika maeneo ya Mkoa wa Kilimanjaro na Arusha huku utabiri ukionyesha kuwepo kwa mvua ya wastani wa Milimita kati ya 50-300. Maeneo mengine yaliyosalia yanatarajiwa kuwa na mvua chache zenye wastani wa chini ya Milimita Kumi (10).