Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Hamidu Aweso kunusuru kaya 730 Wilayani Arumeru Mkoani Arusha
Waziri wa Maji Mhe.Jumaa Aweso (Mbunge) amezindua rasmi mradi wa urejeshaji Mto Nduruma kwenye mkondo wake ili kunusuru makazi 730 yaliyokuwa yakiathiriwa na mafuriko katika Kata za Shambarai Burka na Mbuguni, pamoja na hekari 3,280 za mashamba na barabara 5 zenye jumla ya urefu wa Km 18.
Akizungumza baada ya uzinduzi huo uliofanyika katika Kata ya Shambarai burka Mhe.Waziri Aweso amesema Serikali ya awamu ya Sita ikiongozwa na Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan inahakikisha wananchi wake wapo salama kwani imetoa milioni 250 za mradi huo wa kurejesha Mto kwenye mkondo wake ili kudhibiti mafuriko "Serikali ilisikia kilio chenu na kuleta fedha hizi, nitoe wito kwenu kutokufanya shughuli au kuharibu vyanzo vya maji kwani jukumu la kutunza vyanzo vya maji ni jukumu letu sote " amehimiza Mhe. Aweso
Mhe. Aweso amesema wananchi na viongozi hawana budi kutunza vyanzo vya Maji kwani maji hayana mbadala na kwakuwa ni uai hakuna uai bila maji ambapo amewaagiza Wakurugenzi wa Mabonde yote ya maji nchini likiwemo bonde la pangani kutembelea na kuvitambua vyanzo vya maji kwa kuweka mipaka sambamba na kushirikiana na Maafisa wa mazingira wa halmashauri katika shughuli za mazingira "haipendezi mnaacha watu kupanda mazao kwenye vyanzo vya maji hadi yanakomaa ndio mnayaharibu kwani wakati wanaanza kupanda mlikuwa wapi? " amehoji Mhe.Aweso
Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki Mhe.Dkt.John D. Pallangyo amesema Serikali ya awamu ya sita imeendelea kuwaletea maendeleo Wananchi wa Arumeru kwani changamoto ya mafuriko ilikuwa kikwazo kikubwa hivyo anaishukuru Serikali kuwa sikivu baada ya kuwasilisha kero hiyo na kuikumbushia wakati wa Bunge sasa utekelezaji umeanza. Pia ameishukuru Serikali kutoa takribani Shilingi Bilioni kumi kwaajili ya utekelezaji wa Miradi ya Maji Jimboni humo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti waheshimiwa madiwani wa Kata za Shambarai burka na Mbuguni wameishukuru serikali kwa mradi wa urejeshaji maji ya mto nduruma kwenye mkondo wake kwani ilikuwa ni changamoto ya wananchi wa Kata hizo kwa muda mrefu.
Nao wananchi wa Kata ya Shambarai Burka wamesema msimu wa mvua wanafunzi walishindwa kuhudhuria masomo kutokana na mafuriko hivyo wanaishukuru serikali kwani mradi ukikamilika utasaidia kudhibiti mafuriko " kunawakati tunashindwa kufanya shughuli za kiuchumi hata miezi 3 kutokana na kukatika kwa mawasiliano kwani barabara zinajaa maji "amesema Neema Mungure mkazi wa shambarai burka.
Uzinduzi huo wa mradi wa urejeshaji mto nduruma umehudhuriwa na Mhe.Waziri wa Maji,Mkuu wa Wilaya ya Arumeru na Kamati ya Ulinzi na Usalama ,Mwenyekiti wa Halmashauri ya Meru, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Meru ,Wahe.Madiwani wa Kata ya Shambarai, Mbuguni,na Kikwe , Katibu wa CCM Meru na Viongozi wengine wa Chama,Viongozi na Watumishi wa Bonde la Pangani pamoja na Wananchi wa Kata za Mbuguni na Shambarai.