Majukumu ya Bodi ya Maji Bonde la Pangani ni yapi?
Tathmini ya Rasilimali za Maji
Tathmini ya Rasilimali za Maji katika Bonde la Pangani hufanyika kupitia takwimu za Rasimali za Maji ambazo hukusanywa katika vituo 205 vya ufuatiliaji wa mwenendo wa maji. Vituo hivyo ni 11 vya Maji Chini ya Ardhi, vituo 54 vya mtoni, vituo 6 vya mabwawa, 42 vya mvua, 13 vya Hali ya Hewa, 40 vya Ubora wa Maji na 39 vya kufuatilia mwenendo wa ubora wa Maji. Katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2015 Bodi imefanikiwa kufanya Ujenzi wa vituo 15 vinavyojiendesha wenyewe (5 automatic mini-weather & 10 automatic water level recorder stations) kupitia mradi uliokuwa ukitekelezwa na Bodi ikishirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Idara ya Maafa. Vilevile, ukarabati wa vituo 13 vya mtoni, vituo 10 vya mvua umetekeelzwa. Aidha, upimaji wa wingi wa maji (flow measurements) umetekelezwa mara 71 katika vituo 54 vya Mitoni na ukusanyaji takwimu za kina cha maji (water levels) umeendelea katika vituo hivyo mara mbili kwa siku. Vilevile takwimu zimekusanywa kila siku katika vituo 42 vya mvua, vituo 13 vya hali ya hewa na vituo 3 vya maziwa na vituo 3 vya mabwawa. Takwimu zinazokusanywa hutumika katika kusanifu miradi ya barabara, madaraja, umeme wa maji, ujenzi wa majengo n.k. Vilevile, takwimu hizo hutumika kuandaa taarifa mbalimbali na kusambazwa kwa wadau pamoja na kutoa tahadhari kwa kuhusu mafuriko hasa kwa wadau wanaoishi maeneo ya pembezoni na upande wa chini wa miundombinu ya kuhifadhi maji kama vile Bwawa la Nyumba ya Mungu ambapo huwasilishwa kwa kutumia barua, simu na vyombo vya habari.
Ugawaji wa Maji
Ugawaji wa Maji katika Bonde la Pangani hufanyika kwa kutoa vibali vya matumizi ya Maji ikiwa ni idhini inayotolewa kisheria na Bodi ya Maji Bonde la Pangani kwa mamlaka iliyokasimiwa na Mhe. Waziri mwenye dhamana ya Maji kwa kufuata Kifungu Na. 43 cha Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Na. 11 ya 2009 ambacho kinamtaka mtu yeyote anayetaka kuchukua maji kutoka katika chanzo cha maji kupata kibali kutoka Bodi ya Maji Bonde la Pangani. Mpaka June 2021, Bodi imefanikiwa kutoa jumla ya vibali 1520 kwa wateja wanajumuisha watu binafsi, taasisi za Serikali kama vile Mamlaka za Maji, viwanda, mashamba n.k. Vibali vilivyotolewa vimewezesha wadau wakiwemo wananchi kuwa na haki ya kutumia maji kwa kuzingatia Sheria na kuvitumia vibali hivyo katika shughuli za kiuchumi kama vile kilimo cha mbogamboga na kuwawezesha wahusika kukopesheka katika taasisi za fedha. Kutumika kwa vibali hivyo kunasaidia kuwa na uwiano mzuri wa mgawanyo wa maji baina ya watumiaji na hivyo kuepusha migogoro baina ya watumiaji wa maji.
Uhifadhi wa vyanzo vya Maji
Uhifadhi wa vyanzo vya Maji hufanyika kwa kushirikiana na Jumiya za Watumia Maji pamoja na wadau wengine hasa Halmashauri 24 ziliopo katika eneo linalosimamiwa na Bodi ya Maji Bonde la Pangani, taasisi zisizo za kiserikali na waanchi kwa ujumla ambapo huanza na ubainishaji maeneo ambayo ni vyanzo vya maji na baadae mipango ya pamoja huandaliwa katika kuhakikisha kuwa vyanzo hivyo haviharibiwi ambayo huhusisha uwekaji wa alama za kudumu (beacons), usimikaji wa mabango ya makatazo ya shughuli za kibinadamu pamoja na upandaji na ukuzaji wa miti rafiki na vyanzo vya maji. Kupitia ushirikiano huo jumla ya vyanzo 700 vimebainishwa katika maeneo mbalimbali ya Bonde, alama za kudumu 1823 zimewekwa katika vyanzo 20, mabango ya makatazo 161 pamoja na miti rafiki na Maji 30,000 imepandwa katika vyanzo vya maji. Mafanikio katika eneo hili yanategemea sana uelewa wa wananchi hivyo Bodi huwekeza katika kutoa elimu kwa wananchi kupitia Jumuiya za Watumia Maji 23 ziliopo ndani ya Bonde la Pangani.
Usimamizi endelevu wa Rasilimali za Maji
Usimamizi endelevu wa Rasilimali za Maji katika Bonde la Pangani hufanyika kwa kuzingatia mfumo shirikishi unaotoa fursa kwa jamii katika kupanga na kusimamia matumizi ya maji kama ulivyoainishwa katika mageuzi makubwa ya sekta ya Maji yaliyofanyika kupitia Sera ya Maji ya Mwaka 2002. Kufuatia maelekezo hayo ya ki-sera, sehemu ya VIII ya Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Na. 11 ya Mwaka 2009 imeelekeza kuundwa kwa Jumuiya za watumia maji ambazo zimepewa majukumu ya kuhakisha vyanzo vya maji vinasimamiwa ipasavyo katika ngazi ya Jamii ambapo Jumuiya hizo huundwa kwa kuzingatia Kifungu cha 80 mpaka 83 cha sheria hiyo. Mpaka Juni 2021 Bodi imefanikiwa kuunda na kusajili jumla ya Jumuiya za Watumia 23 pamoja na kamati za vidakio mbili ambazo zimekuwa ni kiungo muhimu sana kati ya Bodi na jamii katika kuhifadhi vyanzo vya Maji na kupunguza migogoro inayosababishwa na Maji katika Bonde. Pia imeimarisha mfumo huu shirikishi kwa kuongeza fursa muhimu ya kujadiliana kwa pamoja, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya pamoja kwa wadau wa Maji kwa kuanzisha majukwaa ya wadau ambapo mpaka sasa Bodi imeanzisha Jukwaa la Wadau wa Bonde la Pangani pamoja na majukwaa matatu (3) ya vidakio vya Themi, Zigi na Umba. Uanzishwaji wa majukwaa haya umeiwezesha Bodi kutambua fursa na mipango ya wadau ya uhifadhi wa vyanzo ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza kasi ya kutimiza lengo mahsusi la kuhakikisha kuwa vyanzo vya maji vinatunzwa na kuongeza upatikanaji endelevu wa Maji katika Bonde la Pangani.
Bodi inasimamia eneo la Kilomita za Mraba zipatazo 54,600 ikijumuisha maeneo ya vyanzo ambayo mengi yako mbali na miji. Kwa kuzingatia ukubwa wa eneo ambalo Bodi inalisimamia ushirikiano wa karibu na Jumuiya za Watumia Maji na Ofisi za Serikali za Mitaa na Vijiji ni jambo muhimu sana.